SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 6 Aprili 2016

T media news

Serikali isiyotambuliwa kimataifa Libya yakabidhi madaraka


Serikali isiyotambuliwa kimataifa Libya yakabidhi madaraka
Serikali isiyotambuliwa kimataifa ya Tripoli nchini Libya imetangaza kuwa imekabidhi madaraka kwa serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Serikali hiyo yenye makao yake mjini Tripoli jana jioni ilitangaza kuwa, imekabidhi madaraka kwa serikali ya umoja wa kitaifa ili kutayarisha uwanja mzuri wa serikali ya maridhiano ya kitaifa. Serikali hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Khalifa al-Ghweil inadhibiti mji mkuu wa Libya na maeneo mengi ya magharibi mwa nchi hiyo kwa msaada wa makundi yawanamgambo wa Fajr Libi tangu mwezi Agosti mwaka 2014. Imesema imesitisha shughuli zake zote za kiutendaji. Taarifa ya serikali hiyo imesema uamuzi huo umechukuliwa kwa shabaha ya kuzuia umwagaji damu na kuzuia machafuko na kugawanywa nchi.
Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Faiz al Siraj na baraza lake la mawaziri waliwasili katika mji mkuu wa Libya, Tripoli tarehe 30 Machi akitokea Tunisia. Baada tu ya serikali hiyo kuwasili Libya, serikali na bunge lisilotambuliwa kimataifa la Tripoli liliitaka seikali ya umoja wa kitaifa kujiunga nayo au kuondoka Tripoli. Kwa msingi huo uamuzi wa serikali ya Tripoli wa kukabidhi madaraka kwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa ni hatua muhimu katika mwenendo wa kurejesha amani ya kudumu nchini Libya.
Libya inaendelea kusumbuliwa na machafuko na mapigano ya ndani yaliyoanza baada tu ya kuondolewa madarakani serikali ya kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Hitilafu za ndani kwa upande mmoja na kusonga mbele kwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh na kuteka sehemu kubwa ya maeneo yenye utajiri wa mafuta kwa upande mwingine, bila ya kusahau mashindano ya madola makubwa na baadhi ya nchi za Kiarabu zinazochochea machafuko ya ndani na kuyafadhili kwa silaha makundi hasimu ya Libya, vimekuwa vikiisukuma zaidi Libya upande wa kugawanyika. Hata hivyo kwa sasa inaonekana kuwa makundi hasimu ya Libya yametambua hatari inayoikabili nchi hiyo na kuamua kuipa nguvu serikali ya umoja wa kitaifa kama hatua ya kwanza muhimu ya kurejesha amani kamili nchini humo.
Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, changamoto kubwa zaidi ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ni kurejesha amani na usalama nchini humo na kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh. Hii ni kwa sababu siku kadhaa zilizopita bu Abdullah al-Misri, kiongozi wa genge hilo la kigaidi mwenye makao yake mjini Sirte, ametishia kufanya shambulio dhidi ya serikali hiyo mpya na ameitaja serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kuwa ni 'serikali ya kimsalaba'.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kutokana na utajiri mkubwa wa mafuta wa Libya baadhi ya nchi za Magharibi na hata za Kiarabu zinafanya mikakati ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa ajili ya kudhamimi maslahi yao, kwa msingi huo serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inapaswa kuwa macho zaidi mbele ya njama hizo za kigeni.
Alaa kulli hal, japokuwa kazi ya kurejesha amani na usalama kamili nchini Libya na kuyaangamiza makundi ya kigaidi ni kibarua kigumu na kinachohitajia muda wa kutosha lakini inaonekana kuwa, inawezekana kutimizwa lengo hilo kwa ushiikiano wa makundi yote ya kisiasa ya Libya.