SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 23 Machi 2016

T media news

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Champongeza Dk Ali Mohammed Shein Kwa Ushindi wa Kishindo Alioupata



Baada ya Dk Ali Mohammed Shein kutangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 90, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatma ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaamuliwa na Rais kwa kufuata matakwa ya Katiba ya Zanzibar.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Waride Bajari Jabu alisema Dk Shein ataongozwa na Katiba ya Zanzibar pamoja na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mkutano huo ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kumpongeza Dk Shein kuchaguliwa tena kwa mara ya pili na wananchi wa Zanzibar, Jabu alisema maelekezo yote ya kuundwa kwa SUK yamefafanuliwa kikatiba.

Alisema CCM inaamini kuwa katiba ndiyo msingi wa uendeshaji wa nchi, hivyo jambo ilo wanaliachia liamuliwe kwa kufuata matakwa husika ya Katiba ya Zanzibar.

“Rais ataunda serikali yake kikatiba, imefafanua kila kitu,” alisema Jabu wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari. 

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 inataka Serikali inayoundwa iwe ya umoja wa kitaifa kwa kuwa na Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye anatoka chama kikubwa cha upinzani na Makamu wa Pili wa Rais anayeteuliwa kutoka katika miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, CCM imeshinda majimbo yote ya uchaguzi kutokana na hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza kutoshiriki katika uchaguzi huo wa marudio.

Dk Shein alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 91.4 na mgombea aliyemfuatia ni wa ADC, Hamad Rashid Mohamed aliyeambulia asilimia tatu ya kura zilizopigwa.

Kutokana na kutokuwepo mgombea urais aliyepata zaidi ya asilimia 10 ya kura za urais na kutokuwepo kwa chama kilichoingiza wajumbe wengi Baraza la Wawakilishi, CCM imejikuta inabaki pekee yenye sifa zote kikatiba.

Jabu pia alituma salamu za pongeza kwa Dk Shein kwa kuchaguliwa tena kuwatumikia Wazanzibari kwa kipindi cha miaka mitano.

Akitoa salamu hizo, Jabu alisema ushindi wa Dk Shein umedhihirisha namna Wazanzibari wanavyoridhishwa na utendaji kazi wake ikiwa ni pamoja na kumuamini kwao.
Kwa upande wao, Umoja wa Vijana (UVCCM) umesema ushindi alioupata Dk Shein ni kielelezo cha kuimarika kwa msingi ya demokrasia Zanzibar na kukubalika kwa mgombea huyo kwa wapiga kura na wananchi wa Zanzibar.

Kaimu Katibu Mkuu alisema aina ya uongozi wa Rais Dk Shein ni wa kipekee na kwamba kama angekuwa si mtawala mwenye maarifa mapana na uvumilivu wa kisiasa serikali hiyo anaamini ingevunjika mapema