SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 18 Novemba 2017

T media news

TANESCO yatangaza siku mbili za kukatika kwa umeme nchini

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza kuwa kwa muda wa siku mbili baadhi ya maeneo nchini yatakosa umeme baada ya kuzimwa kwa mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi one.

Meneja wa Mradi wa Kinyerezi One, Mhandisi Stephen Mmanda amesema kuwa mtambo huo unazimwa ili kupisha zoezi la kusafisha bomba la gesi pamoja na kuunga bomba jipya katika mitambo hiyo.

“Kuna kazi ya kusafisha bomba la gesi kuja Kinyerezi namba moja kwa ajili ya kuunga bomba jipya la gesi kwa mitambo hii ya Kinyerezi namba moja na vile vile ni maandalizi ya bomba kwa ajili ya kinyerezi namba mbili ambayo tunatarajia kuiweka kwenye gridi ya Taifa hapo mwezi Disemba,” alisema Mhandisi Mmanda.

Aidha aliongeza kuwa kutokana na sababu za kiusalama pamoja na hatari ya zoezi hilo, ndege zote hazitotakiwa kupita katika anga la Kinyerezi na wananchi wote  wa maeneo yanayouzunguka mtambo huo, wametahadharishwa kutowasha moto ama vitu vinavyoweza kusababisha moto.

“Kwa hiyo kazi hii ni kazi ambayo inahitaji usalama wa hali ya juu kwa hiyo mitambo yote ya Kinyerezi namba moja imezimwa na kwa ajili ya usalama vilevile tumetoa taarifa kwenye viwanja vya ndege, kwamba ndege zisiruke kwenye anga hili la Kinyerezi lakini pia kwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu tumewatahadharisha wasichome moto ama kuwasha kitu chochote ambacho kinaweza kusababisha moto,” alisema.