SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 1 Januari 2017

T media news

Rungwe aitaka Serikali isifanye biashara

Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 kwa tiketi ya Chaumma, Hashim Rungwe ameitaka Serikali isijiingize katika biashara, bali iachie sekta binafsi na yenyewe kubaki ikisimamia na kuwezesha.

Akizungumza na ofisini kwake juzi, Rungwe alisema haoni mantiki kwa Serikali kufanya biashara wakati haina msimamizi na hiyo ndiyo iliyosababisha mashirika ya umma na kampuni nyingi kufa.

“Mtu atajitoa vipi kimasomaso wakati anajua mshahara wake unaingia, amekuja kazini sawa asipokuja sawa, mshahara wake uko palepale, sasa hii katika biashara haitakiwi, haya yafanywe na wafanyabiashara Serikali ibaki kuwezesha,” alisema Rungwe.

Akitolea mfano sekta mbalimbali za biashara ikiwamo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Rungwe alisema Serikali imekosea kujitumbukiza kwenye biashara ya ndege kwa kuwa si kipaumbele cha Watanzania.

“Mfano, mimi juzi nilikwenda Zanzibar, nilipanda (anaonyesha tiketi ya shirika moja)... tulikuwa abiria watatu, sasa hii ni hasara, unanunua ndege tano, haiwezekani.

“Serikali iache kujiingiza kwenye biashara, Serikali haifanyi biashara inasaidia miradi mikubwa. Duniani kote sekta za reli, mambo makubwa makubwa ni watu binafsi.

“Sisemi isifanye biashara na isiwe nchi ya viwanda, lakini wanaotakiwa kuwa na viwanda ni raia na si NSSF (Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii) wachukue hela waanzishe viwanda bado sikubaliani,” alisema Rungwe ambaye pia ni wakili na mwanasheria. Rungwe aliyeshika namba tano kwenye uchaguzi wa 2015, alisema wakati Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi anaingia madarakani, viwanda vyote vilishakufa na bila watu kuja nchini kufanya biashara, viwanda visingekuwapo.

“Tukianza kusema Serikali iwawezeshe Watanzania bila kuwashirikiana na watu wa nje ni kuwakatisha tamaa wenzetu wa nje, wale ni wenzetu tunatakiwa kuwakaribisha ili kujifunza kutoka kwao, tusianze kuonyesha uadui lakini ninasema, Serikali ikijiingiza moja kwa moja kwenye biashara, tutarudi palepale,” alisisitiza.

Serikali kubana vyama vya upinzani
Kuhusu Serikali kuzuia vyama vya upinzani kufanya siasa, alisema: “Kwanza ninavipongeza vyama upinzani kwa ukomavu wa kisiasa, wametii amri na busara kuendelea kulinda amani yetu kwa kuwa sisi ni wasikivu nikiwamo na mimi.”

Alisema wapinzani waliwaambia wapigakura wao kuwa wafanye subira na waendelee kumuomba Mungu alete mabadiliko yanayotokea.

Rungwe alisema walikuwa na matarajio makubwa kwamba baada ya uchaguzi wangezunguka nchini nzima kuwafikia wananchi bila ya kuvuruga amani ya nchi.

“Navipongeza vyama vya siasa kwa kuonyesha ukomavu, walipanga kuzungumza na wananchi, lakini askari wakaandaliwa kupambana na wanasiasa, wao wameandaliwa kwa ajili ya kupambana na adui, tukakaa tukasema tusishindane nao wana nguvu ya mabomu na silaha.

“Tulitarajia baada ya uchaguzi tujipange kufanya siasa, kuongeza wanachama, kufungua matawi kila mahali, lakini tumepigwa marufuku hadi 2020 sasa kama sionekani majibu yapo, tumezuiwa kufanya siasa,” alisema.

Alisema kwa sasa kuna mtindo watu kukutana kwenye ofisi za vyama na kwamba hilo si la leo na si jipya.

“Tulikuwa tunakutana na wala hakukuwa na vibali, lakini leo hii inakuwa issue! Watu wanakutana wanafanya uchaguzi ndani, wanaelezana siasa ndani, hii si fursa, fursa ni kutoka mbele ya wananchi kuwaambia siasa, afadhali ingeelezwa kuwa baadhi ya vipengele vya kisheria kuhusu mikutano vimefutwa.