Wanasayansi wa afya ya jamii wanaonya kuwa michoro iliyotokana na rangi za madukani pamoja na vichoreo vyake, vinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa wahusika.
Watu wengi, wanaume kwa wanawake hupenda kuweka michoro mwilini kama mapambo yaani tattoo au namna fulani ya kiimani.
Baadhi ya rangi zinazotumika kuchora mapambo mwilini zinaweza kusababisha mzio wa ngozi katika eneo la mwili mahali palipo na tattoo. Mzio huu unaweza kutokea kipindi kirefu baada ya kuchora tattoo.
Tafiti nyingi za kitabibu pia zinaonesha kwamba, wino au rangi za tattoo zinaweza kusababisha uambukizo wa bakteria aina ya Mycobacterium cholonae.
Bakteria hawa wanaweza kusababisha magonjwa ya ngozi na nyama za mwili, matatizo ya njia ya mkojo, mfumo wa kupumua, magonjwa ya uambukizo kwenye mifupa na nyama za moyo.
Michoro hiyo pia huweza kusababisha homa ya uti wa mgongo na tatizo la macho.
Vilevile, vifaa vinavyotumiwa kuchora mapambo hayo hutumika kwa watu mbalimbali kwa wakati mmoja bila utaalamu sahihi wa kuvisafisha.
Hali hiyo huweza kusababisha vibebe vimelea vya magonjwa mbalimbali na kuyahamishia kwa wengine.
Hali hii inaweza kusababisha uambukizo wa magonjwa yatokanayo na virusi hatari kama vile virusi vya Ukimwi, virusi ninavyosababisha homa ya ini (Hepatitis B na C) au virusi vya malengelenge (herpes simplex virus).
Kumbuka, wakati wa kuchora tattoo, ngozi hutobolewa kwa mashine au sindano hadi kuifikia sehemu ya ndani kabisa. Hii ni hatari kwa afya yako.