SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 8 Septemba 2017

T media news

Zawadi ya Almasi ya Sh450 Bilioni Yaibua Mjadala....Kamati Yashindwa Kumtaja Kiongozi Aliyepewa Zawadi

Mwenyekiti wa kamati maalum iliyoundwa kuchunguza biashara ya almasi, Mussa Azzan Zungu alikuwa na ujasiri wa kutangaza zawadi ya thamani ya takriban dola 200 milioni za Kimarekani, lakini akachelea kumtaja aliyepewa badala yake akasema “kiongozi mmoja wa juu wa zamani”.

Sasa, kitendo cha kutomtaja kimeamsha mjadala kutokana na baadhi ya watu kutaka kujua jina la aliyepewa zawadi hiyo, huku wengine wakiibua suala la kuandikwa kwa Katiba mpya kuwa ndio litaondoa usiri kama huo.

Akisoma ripoti ya kamati yake, Zungu alisema kuna wakati kiongozi mmoja wa wa juu alipewa zawadi ya madini na mgodi mmoja, na kwamba thamani ya madini hayo kwa sasa ni takriban dola 200 milioni (sawa na Sh450 bilioni za Kitanzania), lakini hakufafanua wala kutaja jina la aliyepewa.

Wadau waliohojiwa na Mwananchi jana walikuwa na hisia tofauti kuhusu kitendo hicho, baadhi wakisema kamati ingeweza kumtaja lakini asichukuliwe hatua kama wengine huku baadhi wakitaka Katiba mpya iandikwe ili kunyoosha mambo.

“Inawezekana kamati haijamtaja kigogo huyo kutokana na kilichopo kwenye Katiba,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse, akirejea mazuio ya Katiba kuhusu viongozi wakuu.

Alisema inawezekana wameona hata wakilitaja jina lake, hawezi kushitakiwa wala kuhojiwa ndiyo maana wamesema kigogo.

Alisema hakuna aliyeko juu ya sheria, lakini kwa Katiba inayotumika sasa, kuna viongozi wapo juu.

“Kama ukweli na uwazi unaonadiwa sasa ambao kila mmoja anataka ufanye kazi kama inavyokusudiwa, inabidi Katiba mpya itayarishwe,” alisema.

“Lakini kwa hii Katiba iliyopo uwazi utabaki kwa baadhi ya watu, huku wengine wakiendelea kufanya wanachokitaka, tena wakiwa na uhakika kuwa hakuna wanaloweza kufanyiwa sasa na hata baadaye.”

Kwa upande wa Profesa Bakari Mohamed alisema kama kamati hiyo ina nia ya kutokomeza lililobainika ili lisijirudie, kuna haja ya kuliweka hadharani jina la kigogo huyo.

Alisema ingawa bado ni mtuhumiwa na ana nafasi ya kuhojiwa ili kuthibitisha, kama ni kiongozi wa juu itabaki kuwa siri kwa sababu Katiba imeelekeza hivyo.

Alisema kutotaja jina la aliyepewa madini hayo, kunamaanisha kamati imefanya kazi nusu na inatakiwa imalizie.

Lakini Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) alizungumzia taratibu za zawadi, akisema kwa watumishi wa umma zawadi ikizidi Sh50,000 lazima iwe bayana na aliyepewa aeleze wazi.

Alisema kama huyo kigogo hakuweka wazi, anakuwa mtuhumiwa na anastahili kutajwa kama walivyotajwa wengine.

Alisema ili kukwepa mambo kama hayo ndiyo maana kuna haja ya kuwa na Katiba isiyowapa kinga viongozi wakubwa wanaoitwa majina kama hayo ya kigogo wa serikalini.

Alisema ili uwe kigogo wa serikalini, lazima uwe ni mtumishi wa umma na uwatumikie wananchi badala ya kuwa juu ya sheria, lakini kwa katiba ya sasa hao vigogo wasiotajwa ni kama wapo juu ya sheria.

Alisema ni vigumu kwa waziri kusaini mikataba mikubwa bila ya viongozi wake wa juu kuhusishwa.

Mpangala alishauri kuwa kamati ingemtaja jina muhusika, halafu kinga yake ikafanya kazi kumlinda ili wananchi wajue nini kinaendelea.

“Hii siyo sawa, kama wengine wametajwa huyo asiyetajwa ni nani?” alihoji.