SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 9 Septemba 2017

T media news

Ni ngumu washambuliaji wa Simba kuifunga Azam FC yenye beki ya kimataifa

Na Baraka Mbolembole

SIMBA SC inahitaji safu ya mashambulizi kujiamini dhidi ya safu ya ‘ulinzi ya kimataifa’ ya Azam FC wakati timu hizo zitakapopambana katika wiki ya pili ya ligi kuu Tanzania bara msimu huu. Simba wamefunga magoli saba katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Uhuru, lakini ni goli moja tu ambalo lilifungwa na mshambulizi ‘asilia’ Juma ‘Ndanda’ Liuzio.

Kiungo-mshambulizi, Emmanuel Okwi alifunga magoli manne katika ushindi wa timu yake vs Shooting, Shiza Kichuya, na mliinzi ‘kiraka’ Erasto Nyoni kila mmoja alifunga goli moja.

Okwi ndiye anayeongoza chati ya ufungaji bora msimu huu kwa magoli yake manne, labda kocha Mcamerron, Joseph Omog anaweza kumtumia mshambulizi huyo wa Uganda katika nafasi ya mshambulizi wa kwanza, huku Kichuya na Mohamed Ibrahim wakicheza kama washambuliaji wa pembeni ili kupata safu ya mashambulizi yenye ubunifu ili kuwapita walinzi imara wa Azam FC.

Beki ya Azam ni ngumu kwa washambuliaji wa Simba

Golikipa raia wa Ghana, Razak Abalora anataraji kukutana na mashambulizi mengi katika mchezo wa Jumamosi hii kama tu atashindwa kuwapanga walinzi wake. Kipa huyo alionyesha kiwango kizuri katika mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu Bara vs Ndanda FC katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara.

Razak alimaliza dakika 90’ akiwa mshindi kwani timu yake ilifanikiwa kushinda 1-0. Aggrey Morris anaweza kuwa mchezaji pekee wa Kitanzania ambaye ataanza katika safu ya walinzi watatu (kama kocha Mromania, Aristica Cioaba ataamua kubaki katika mfumo alioutumia dhidi ya Ndanda) Mcameroon, Yakubu Mohamed na Mghana, Daniel Amoah walianza kama walinzi watatu-pacha katika mfumo wa 3-4-3 lakini mfumo huo ulishindwa kufanya kazi vizuri dhidi ya Ndanda.

Mzimambwe, Bruce Kangwa aliungana na viungo, Yahya Zayd, Frank Domayo na Salum Abubakary na kutengeneza safu ya walinzi wanne. Mfumo wa 3-4-3 hautafaa kwa Azam FC vs Simba kwa maana watakubali kushambuliwa sana jambo ambalo linaweza kuwapa ‘miaya’ viungo washambuliaji wa Simba ikiwa kocha Omog ataanza kwa kumpanga Okwi kama mshambulizi wa kwanza.

Aristica anapaswa kubadilisha mfumo, kuwapanga Agrey, Yakubu, Amoah na Kangwa kama walinzi wanne wa kwanza itakuwa jambo zuri kwake kwani atakuwa na walinzi wa kutosha ambao wanaweza kutumia uzoefu wao kuisogeza mbele timu pale inapohitajika.

Walinzi hawa wanne wanaweza kuwazima Simba katika ‘ujio wao wowote’ iwe, John Bocco, Liuzio, Mavugo ama Okwi na kundi lake wote watasumbuka sana kuipita beki hii kwa sababu washambuliaji wote wa Simba wapo katika ‘maji marefu’ kiufungaji.

Pia wanne hawa wanaweza kumpa fursa pana Aristica kutumia mifumo mingine tofauti, 4-5-1 kama ataamua kucheza mchezo wa tahadhari na kutegemea eneo la kiungo kushinda mechi. Ama Mromania huyo anaweza kutumia 4-3-3 kama ataamua kushamblia, ama 4-4-2 ambao pia utawapa Azam nguvu kubwa katika kila idara.

Himid, Zayd, Domayo, Sure Boy ni sahihi katika 4-4-2 

Kuwapanga viungo hawa wanne mbele ya Agrey, Yakubu, Amoah na Kangwa kutaifanya Azam FC kwenda mbele huku ikiwa na nguvu kubwa katikati ya uwanja. Himid anaweza kuzunguka na kuficha njia zote za Haruna Niyonzima. Na ili kuifanya Simba kushindwa kushambulia sana, Azam wanapaswa kwanza kujua namna ya kumzima nohodha huyo wa Rwanda. Kazi hii anaiweza vizuri nahodha wa kikosi, Mao.

Yahya Zayd ni kijana mwenye miaka 19 tu, lakini ikiwa atapewa nafasi ya kuanza katika mfumo huu itakuwa kazi ngumu kwa Erasto Nyoni ama Mohamed Hussein. Kijana huyu ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga krosi-pasi, kukokota mpira na mwenye uamuzi wa haraka. Inaweza kuwa kamari kuanza na kijana huyu lakini  dakika zaidi ya 80 alizocheza vs Ndanda zinaweza kuondoa wasiwasi wote kwa kocha wake Aristica na si ajabu akaibeba timu yake.

Frank Domayo ana kawaida ya kucheza ‘katika eneo lake’ na kitendo cha kiungo huyo kuwa na uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia haraka kwa pasi ndefu ni sawa na kuwa na viungo wawili ambao watakuwa na majukumu tofauti uwanjani. Domayo atamsaidia sana Himid katika ukabaji wakati huohuo atakuwa msaada wa kumfanya Sure Boys kumnyima uhuru wa kuanzisha mashambulizi ya Simba, Mghana wa Simba, James Kotei.

Sure Boy ni mchezesha timu mzuri, lakini tatizo lake anapendelea sana kucheza pasi za pembeni. Pasi zake mbili au tatu kwenda eneo ambalo atacheza mshambulizi, Mghana, Yahaya Mohamed na Mbaraka Yusuph.

Beki ya Simba vs wafungaji wa Azam FC

Ally Shomari na Erasto Nyoni wamekuwa wakianza katika beki za pembeni msimu huu katika kikosi cha Simba sehemu ambazo zilikuwa zikichezwa na Mcongoman, Besala Bokungu na nahodha msaiidizi wa kikosi hicho, Mohamed Hussen ‘Zimbwe Jr’ Shomari amekuwa akishambulia vizuri akitokea katika beki namba mbili. Erasto yeye amekuwa akizuia vizuri.

Nahodha wa Simba, Mzimbabwe, Method Mwanjali anaweza kuanza sambamba na Salim Mbonde kama kocha wao Omog hatabadili kikosi chake ambacho kilianza vs Shooting. Walinzi hao wanne wanaweza kusumbuliwa sana na mbio za Mghanga, Yahaya ambaye tangu kuanza kwa michezo ya kujiandaa kwa msimu amekuwa akifunga.

Mohamed alifunga goli pekee la Azam FC wakati walipoichapa Ndanda FC siku ya ufunguzi wa msimu. Mbaraka Yusuph  alicheza kwa dakika zisizopungua 30 katika mchezo huo baada ya kuingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Mohamed. Sasa naona wawili hao wanaweza kuanza pamoja katika safu ya washambuliaji wawili vs Simba ama watatu ikiwa Aristica ataanza na mfumo wa 4-3-3.

Wazir Junior pia anaweza kuwa chaguo lingine bora katika safu ya washambuliaji wa Azam FC na kitendo cha washambuliaji hao wote kuwa fiti itakuwa ni sawa na kuipima sasa safu mpya ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na golikipa wa zamani wa Azam FC, Aishi Manula.