SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 8 Machi 2017

T media news

‘Kama vipi Sanchez asepe tu’ – Madee

Juzi kati hapa liliibuka sekeseke kati ya kocha wa Arsenal na Alexis Sanchez ikisemekana wawili hao walipishana maneno kitu kilichopelekea Sanchez kuanzia benchi kwenye mchezo wa Premier League wakati Arsenal ikicheza na Liverpool.

Wakati game hiyo ikiendelea, Sanchez akiwa kwenye benchi alionekana akicheka wakati timu yake tayari ikiwa nyuma kwa magoli mawili dhidi ya Liverpool. Tukio kama hilo (kucheka) limetokea tena kwenye mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya Arsenal vs  Bayern Munich.

Inasemekana Sanchez hana furaha ndani ya Arsenal na anataka kuondoka kwa sababu timu hiyo ya London haijaonesha ubavu wa kuwania mataji makubwa kama ligi na klabu bingwa Ulaya.

Msanii Madee ambaye ni shabiki wa ‘kutupwa’ wa Arsenal yeye kwa upande wake amesema hana kinyongo na Alexis Sanchez ikiwa ataamua kuachana na Arsena na kuelekea anakotaka yeye kwa sababu tayari ameifanyia makubwa klabu na anahitaji mataji kitu ambacho hawezi kufanikiwa akiendelea kubaki Arsenal kwa sababu hakuna wachezaji wa kiwango chake watakaosaidiana kutwaa mataji.

“Kwa upande wangu mimi, sioni kama Sanchez anakosea anapotaka kuondoka kwenda sehemu nyingine. Mchezaji kama yule anatamani kuwa na mataji kwa sababu marafiki zake wengi ambao walianza soka pamoja, wameshabeba mataji tofauti na yeye anakiu kwa sababu wakati anakuja Arsenal alikuwa anawaza kubeba makombe lakini kama anakosa hicho kitu na kuamua kuondoka ni vizuri kumuacha aende.”

“Ameshatutumikia vizuri na kuonesha nidhamu nzuri, amecheza kwa asilimia zote ambazo tulihitaji lakini hakuna wachezaji wa kiwango chake wa kumsaidia ili kuchukua makombe, kwa hiyo kama anataka kwenda sehemu nyingine kwa upande wangu wamuache andelee na maisha yake mengine sina tatizo na Sanchez.”

“Tunashukuru kwa alichokifanya akiwa Arsenal.”