Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) imeamua kwamba Tanzania ilikiuka baadhi ya haki za wanamuziki Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza 'Papii Kocha' katika kesi ambapo wawili hao walikuwa wamehukumiwa kufungwa jela maisha.
Wawili hao waliwasilisha rufaa katika mahakama hiyo mwaka 2015 kupinga hukumu ya kifungo cha maisha iliyokuwa imetolewa dhidi yao.
Majaji wa mahakama hiyo wamesema haki zao zilikiukwa kwa kutowapa taarifa za mashahidi wa upande wa mashtaka na kwamba mashahidi hao hawakuhojiwa mahakamani.
"Mahakama inatambua kwamba taifa lililoshtakiwa halijapinga madai kwamba walalamishi hawakupewa taarifa za mashahidi na kwamba mashahidi wanne hawakuitwa kuhojiwa," majaji wamesema.
Majaji hao wamesema kila mshtakiwa ana haki ya kupata muda wa kutosha na rasilimali za kutosha kujiandaa kujitetea.
Aidha, kila mshtakiwa ana haki ya kuwahoji mashahidi waliowasilishwa dhidi yake.
"Katika kesi hii, walalamishi wangepewa nakala za mashahidi wa mashtaka kuwawezesha kujiandaa kujitetea. Kwa hili kutofanyika, waliwekwa katika hali iliyowabana ukilinganisha na upande wa mashtaka, kinyume na kanuni ya usawa wa nguvu ya silaha.
"Aidha, kwa kutowaita mashahidi hao wanne watoe ushahidi mahakamani, walinyimwa fursa ya kuwauliza maswali, na hili liliwaweka katika nafasi iliyowabana."
Majaji walisema hilo lilikuwa ukiukaji wa Kifungu cha 7 (1c) cha Mkataba unaounda mahakama hiyo kwa upande wa serikali ya Tanzania.
Hata hivyo, mahakama hiyo imesema madai ya wawili hao kwamba haki zao zilikiukwa wakati wa kutambuliwa hayana msingi.
Aidha, mahakama haikupata ukiukaji wowote wa haki kwa kukataliwa kwa ushahidi wao kuhusu eneo walipokuwa wakati wa kutekelezwa kwa uhalifu huo.
Kuhusu kwamba matokeo ya kupimwa mkojo na damu hayakuwasilishwa, mahakama hiyo imesema haki zao hazikukiukwa kwani matokeo hayo hayakutumiwa na Mahakama Kuu wala Mahakama ya Rufaa kuamua kwamba walikuwa na hatia.
Hata hivyo, kuhusu ombi la mmoja wa washtakiwa apimwe uwezo wake wa kuzaa, mahakama hiyo imesema Tanzania ingefanikishwa apimwe.
"Matokeo ya hilo yangebaini iwapo Bw Nguva angetekeleza uhalifu aliodaiwa kutekeleza. Mahakama inaamua kwamba kukataliwa kwa ombi hili, Tanzania ilikiuka haki zake kama zilivyoelezwa katika Kifungu 7 (1c) cha Mkataba unaounda Mahakama hii."
Kupitwa na wakati
Bw Nguva na mwanawe walikuwa pia wamedai jaji alikuwa anabagua lakini Mahakama hiyo imeamua hali kwamba baadhi ya washtakiwa walipatikana bila hatia na mashtaka yakapunguzwa, hiyo ni ishara kwamba kesi hizo ziliangaziwa kwa uzito wake.
"Walalamishi hawajatoa ushahidi wa kutosha kuonesha jaji alikuwa na mapendeleo," majaji hao wameamua.
Walalamishi walikuwa wameomba waachiliwe huru kwenye rufaa yao walipoiwasilisha mwaka 2015 lakini majaji wamesema hilo limepitwa na wakati kwani wawili hao waliachiliwa kupitia msamaha wa rais.
Tanzania imetakiwa "kuchukua hatua zote ziwezekanavyo kurejesha haki za walalamishi."
Walalamishi walikuwa wamewasilisha ombi la uamuzi kuhusu kulipwa fidia lakini majaji wamesema hakuna aliyewasilisha hoja kwa maandishi kuhusu ulipaji fidia.
Walalamishi wametakiwa kuwasilisha hoja yao katika kipindi cha siku 40 nayo serikali ya Tanzania ijibu katika siku 40 baada ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo.
Bw Nguza na mwanaye walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha jela kwa kuwabaka wasichana 10 wa shule waliokuwa na kati ya umri wa miaka 6 na 8 mwaka 2003 na walikuwa wametumikia kifungo cha miaka 13 kufikia wakati wa kupewa msamaha.
Babu Seya ambaye ni miongoni mwa wafungwa 1,821 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika mnamo 9 Desemba, 2017.
Wengine 8,157 walipunguziwa adhabu zao.
Wawili hao ndio walioimba kibao maarufu cha 'Seya' na walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kufungwa maisha au kunyonga ambao walinufaika kutokana na msamaha wa rais.
Hukumu katika kesi yao ilikuwa imepangiwa kusomwa Jumatano wiki hii lakini baadaye ikaahirishwa hadi leo.
Hatua ya Dkt Magufuli kuwasamehea wawili hao ilishutumiwa na watetezi wa haki za watoto na wanawake.
Kate McAlpine, mkurugenzi wa shirika la Community for Children Rights lenye makao yake Arusha aliambia BBC wakati huo kwamba alikuwa "ameshtushwa lakini hakushangazwa" na hatua ya rais huyo. Alisema hatua hiyo ilionesha 'uelewa mdogo' wa kiongozi huyo kuhusu masuala ya udhalilishaji wa watoto.
Nguza Viking na wanawe walipokutana na MagufuliHaki miliki ya pichaIKULU
Image caption
Nguza Viking na wanawe walipokutana na Magufuli
Alilinganisha hatua hiyo na tamko la Rais Magufuli kwamba wasichana wanaoshika mimba hawafai kuwa shuleni.
Matamshi ya Magufuli yawakasirisha wanawake Tanzania
"Huwa hafahamu vyema mambo, hasa yanayohusu watoto kama waathiriwa. Wasichana wanaoenda shule hushika mimba kwa sababu mara nyingi ni waathiriwa wa udhalilishaji," alisema Bi McAlpine.
Ilikuwaje hadi tukafika hapa?
Nguza Viking na Johnson Nguza ni baba na mwanaye na ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao walikuwa wanamuziki Dar es Salaam.
Wote walikamatwa 12 Oktoba, 2003 na kuzuiliwa kituo cha polisi cha Magomeni ambapo baadaye walifikishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu 16 Oktoba, 2003 na kufunguliwa mashtaka 10 ya ubakaji na 11 ya ulawiti.
Waathiriwa wao walikuwa watoto wa kati ya miaka sita na nane, na walikuwa wote kutoka darasa moja.
Waathiriwa hao walidaiwa kubakwa na kulawitiwa kwa zamu na wanaume watano.
Mnamo 25 Juni, 2004 hakimu aliwapata na hatia na kuwafunga jela Nguza na wanawe watatu. Mshtakiwa wa nne, ambaye alikuwa mwalimu, alipatikana bila hatia.
Washtakiwa walikata rufaa Mahakama Kuu lakini rufaa yao ikatupwa.
Walikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa.
Mwaka 2010 rufaa yao ilisikilizwa na 30 Oktoba Majaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati katika Mahakama ya Rufaa wakawaachilia huru Nguza Mashine na Francis Nguza baada ya kuwapata bila hatia.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo iliwashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania, na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo za rhumba, ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na kuwa na mashabiki wengi.