Viongozi wa umoja wa Ulaya wameungana kumuunga mkono waziri mkuu wa Uingereza Theresa May katika kuilaumu nchi ya Urusi kwa shambulio la sumu kusini mwa jiji la London na kukubaliana kumuitisha balozi wao wa Moscow kwa majadiliano zaidi.
Baadhi ya nchi nazo zimeanza kufikiria kuchukua hatua kama za Uingereza za kuwafurusha wanadiplomasia wa Urusi, huku nchi za Lithuania na Ufaransa zikiwa nchi za awali kuonesha kutaka kufanya hivyo.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May aliwaambia wenzake wa umoja wa Ulaya kuwa ni muhimu kuungana kupinga tukio la Machi 4 ambapo jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal na mtoto wake Yulia walipewa sumu iliyowaathiri mishipa ya fahamu kwenye mji wa Salisbury.
Katika mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Brussels hapo jana, viongozi wa nchi 28 wametangaza kuiunga mkono Uingereza na kukubaliana kuwa kuna uwezekano mkubwa utawala wa Moscow ulihusika na kwamba hakuna maelezo mengine yanayoweza kupindisha ukweli.
Viongozi hao wameahidi kuchukua hatua za pamoja na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesema wamekubaliana kumuita balozi wao mjini Moscow kwa majadiliano zaidi.
"Baadhi ya nchi wanachama wanaangalia uwezekano wa kuwafurusha wanadiplomasia wa Urusi kwenye nchi zao au kuwatisha wanadipolomasia wao," imesema taarifa ya umoja wa Ulaya.
Utawala wa Moscow unakanusha vikali madai kuwa ulihusika kwenye shambulio la sumu la London ambapo inadaiwa kuwa sumu aina ya Novichok inayotengenezwa na nchi hiyo ndio iliyotumika.
Waziri mkuu May amewaambia viongozi wenzake kuwa ni lazima ziungane katika kuikemea nchi ya Urusi na kuonya kuwa ikiwa watafumbia macho matendo kama haya, nchi hiyo itaendelea kuwa tishio kwa miaka mingi ijayo.
Jasusi Skripal na mwane bado wako hospitalini wakipatiwa matibabu baada ya kupatikana wakiwa wamezimia kwenye bustani moja ya mapumziko licha ya polisi aliyekuwa ameathiriwa na sumu hiyo wakati akiwahudumia, jana akiruhusiwa kutoka hospitalini.