Serikali jana iliwasilisha bungeni bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 ambapo ilipendekeza kufanya marekebisho ya viwango maalum vya ushuru (specific duty rates) vinavyotozwa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 5. Lakini pia serikali ilifanya mabadiliko kwa mafuta, kama ilivyoanishwa hapo chini.
Kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho hayo. Mabadiliko yaliyopendekeza ni kama ifuatavyo:-
1. Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha shilingi 40 kwa lita moja kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 379 kwa lita kwa mafuta ya petroli, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 255 kwa lita kwa mafuta ya dizeli na kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 425 kwa lita hadi shilingi 465 kwa lita kwa mafuta ya taa.
2. Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita.
3. Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji yanayozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita.
4. Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini (local juices) utashuka kutoka shilingi 9.5 kwa lita na kuwa shilingi 9.0 kwa lita.
5. Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini (imported juices) kutoka shilingi 210 kwa lita hadi shilingi 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
6. Ushuru wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted Cereals) kutoka shilingi 429 kwa lita hadi shilingi 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 21 kwa lita;
7. Ushuru wa Bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka shilingi 729 kwa lita hadi shilingi 765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 36 kwa lita;
8. Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka shilingi 534 kwa lita hadi shilingi 561 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 27 kwa lita;
9. Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka shilingi 202 kwa lita na kuwa shilingi 200 kwa lita;
10. Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 2,236 kwa lita hadi shilingi 2,349 kwaa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita;
11. Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 3,315 kwa lita hadi shilingi 3,481 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 166 kwa lita. Aidha,Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 3,315 kwa lita;
12. Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na 39 tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 11,854 hadi shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 593 kwa kila sigara elfu moja;
13. Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 28,024 hadi shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,401 kwa kila sigara elfu moja;
14. Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (12) na (13) kutoka shilingi 50,700 hadi shilingi 53,235 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,535 kwa kila sigara elfu moja;
15. Ushuru wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 25,608 hadi shilingi 26,888 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,280 kwa kilo; na
16. Ushuru wa Bidhaa wa “cigar‟ unabaki kuwa asilimia 30.