SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 12 Februari 2017

T media news

Minziro amewataja walioipasha Singida United kucheza VPL

Kocha wa Singida United Fred Felix Minziro amesema sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Singida ndio sababu pekee ya timu yao kupanda daraja na kurejea ligi kuu Tanzania bara msimu ujao.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga amesema, malengo waliyojiwekea yametimia kwa kiasi kikubwa baada ya kufanikiwa kupanda kucheza VPL msimu ujao.

“Ushirikiano wa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki ambao wametupa sapoti kubwa kuhakikisha tunapata ushindi. Siri kubwa ya ushindi wetu ni sapoti kubwa tuliyoipata kutoka kwa mashabiki wetu” – Fred Felix Minziro.

“Malengo tuliyokuwa tumejipangia Singida United yametimia katika kiwango kikubwa kwa maana kwamba tumeweza kuifunga timu ngumu kama Alliance japo mechi ilikuwa ngumu.”

Mashabiki wengi waliingia uwanja wa Namfua mjini Singida kushuhudia mchezo wa soka ligi daraja la kwanza kati ya Singida United dhidi ya Alliance kutoka mkoani Mwanza mchezo ambao umeipa nafasi Singida United kurejea ligi kuu Tanzania bara baada ya kusota kwa zaidi ya miaka 10.

Singida United ilipata ushindi wa magoli 2-0, mkongwe Nizar Khalfan alianza kuifungia Singida bao la kuongoza dakika ya 14 baada ya mabeki wa Alliance kuzembea kwa kudhani Nizar alikuwa ameotea.

Kipindi cha pili Singida United wakaandika bao la pili kwa mkwaju wa penati uliopigwa Rashid Gumbo baada ya mchezaji wa Alliance kuunawa mpira kwenye box.

Singida United sasa rasmi wamepanda daraja baada ya Rhino Rangers ambao pia walikuwa na nafasi kulazimishwa sare huko mkoani Kilimanjaro dhidi ya Panone na kuiacha Singida United ifikishe pointi 30 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote ile kutoka kwenye kundi lao.