Na Baraka Mbolembole
WAKATI kikosi cha Mbao FC kitakaposhuka uwanjani kupambana na JKT Ruvu katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza siku ya Jumapili, mafanikio ya klabu hiyo katika michezo 7 ya mwanzo katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu huenda yakawashtua wengi.
Miezi 6 iliyopita, Mbao ilikuwa ikisuasua katika ligi daraja la kwanza huku JKT Ruvu ikiwa katika mashaka ya kubaki VPL. Kwa kipindi hicho mashabiki wengi wa kandanda nchini wangepinga kwamba klabu hizo zinaweza kukutana katika ligi kuu Bara, tena Mbao ikiwa juu ya JKT Ruvu katika msimamo wa ligi.
Kitu ambacho kilikuwa kigumu kukifikiria, sasa kimetokea na Mbao inaamini kwamba inaweza kuwachapa mabingwa hao wa FA Cup 2002.
Ingawa ilipewa ‘kipigo kikali’ na Mbeya City FC, Septemba 3 kwa kuchapwa 4-1 katika uwanja wao wa nyumbani (Kirumba,)
Mbao FC ambayo inashika nafasi ya 7 kwa sasa itakuwa na hamu ya kuonyesha uwezo zaidi kuzingatia kwamba wamefanikiwa kuchukua pointi muhimu kutoka mikononi mwa timu kama Stand United, Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Ndanda FC.
Wamekusanya pointi 5 katika michezo minne ya ugenini (Stand United 0-0 Mbao FC – Agosti 20, Shooting 1-4 Mbao FC – Septemba 17 na Mtibwa Sugar 1-1 Mbao FC – Septemba 24).
Kocha wa timu hiyo, Mrundi, Etienne Ndairagile alisema anahitaji kuaminiwa tu katika kazi yake ili kuimarisha timu hiyo iliyopanda VPL ikiwa na alama 12 tu katika ligi daraja la kwanza.
Mbao ilistahili kuifunga Ndanda FC siku ya Jumanne hii na kupata ushindi wa kwanza wa ligi kuu katika uwanja wao wa nyumbani kwa kuwa wameonesha njia nzuri katika michezo minne waliyocheza ugenini na kupoteza mara moja (African Lyon 3-1 Mbao FC – Septemba 12).
Sidhani kama watafikia ubora ule wa City waliouonesha walipopanda VPL kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14 lakini timu hii ya Mwanza inakuja kwa kasi, inabidi kuwaangalia kwa makini katika ligi ya msimu huu.
JKT Ruvu ipo nyuma ya Mbao kwa alama nne, huku ikiwa na mechi mbili mkononi. Ilipata ushindi wake wa kwanza msimu huu ilipoifunga City 2-0 wikendi iliyopita hii inadhihirisha kikosi chao kinaanza kuamka.
Baada ya kuanza msimu VPL kwa shinda ikipoteza mechi mbili mfululizo katika uwanja wa Kirumba (Mbao FC 0-1 Mwadui FC-Agosti 27, Mbao FC 1-4 City), kisha kipigo kingine kutoka kwa Lyon katika uwanja wa Uhuru kikosi cha Etienne kinaanza kuvutia.
Wanachotakiwa ni kusahau jinsi walivyopanda VPL kwa ‘mbereko’ kufuatia timu tatu zilizokuwa juu yao katika kundi la 3 ligi daraja la kwanza kuteremshwa daraja baada ya kuhusika katika upangaji wa matokeo.
Matokeo yao si mazuri kupita kiasi ila yanadhihirisha, ligi ya msimu huu itakuwa na ushindani mkubwa.